KWAKO KIJANA;
Hii inakuhusu wewe kijana ulieokoka au ambae hujaokoka.tafadhali soma hadi mwisho kwa kutafakari.
Mtume Paulo katika waraka wake kwa Timotheo anamwambia hivi, ‘Mtu awaye yote ASIUDHARAU ujana wako, bali uwe KIELELEZO kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.JITUNZE nafsi yako, na mafundisho yako. DUMU katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo UTAJIOKOA NAFSI YAKO NA WALE WAKUSIKIAO PIA’ (1Timotheo 4:12 & 14).
Sentensi hizi zinatuonyesha kwamba kijana yeyote ambaye amefanya uamuzi wa kuokoka, kwa hakika amefanya maamuzi ambayo yanamtaka amaanishe katika kumfuata kwake Yesu au kuuishi wakovu wake. Pamoja na kumpa Yesu maisha yake ni lazima kijana afanye maamuzi ya kuishi maisha ya kudumu kumpendeza Mungu kwa kuzikubali gharama zinazohusiana na wokovu aliouchagua na si kuishi maisha yenye kupelekea jina la BWANA kutukanwa kama ilivyo kwa baadhi ya vijana wengi leo.
Ukisoma mstari huu wa 1Timotheo 4:14.
Jambo muhimu ambalo Mtume Paulo alikuwa akilisisitiza hapa ni hili; jambo muhimu si tu kumpokea Yesu kama Bwana na mwokozi wako, bali kila mwamini ana kazi kubwa ya kufanya ili KUULINDA NA KUUTUNZA WOKOVU WAKE.
Moja ya changamoto kubwa sana ambazo zinawakabili vijana wengi waliokoka leo ni kuipenda dunia. Kuipenda dunia kumekuwa tanzi kwa vijana wengi na kwa sababu ya kuipenda dunia;
(a) Mahusiano ya vijana wengi na Mungu wao yameharibika
(b) Maisha ya vijana wengi yamekosa uelekeo
(c) Kutokana na uovu wao jina la Bwana Yesu limekuwa likitukanwa.
Katika kile kitabu cha 1Yohana 2:16 ni dhahiri kwamba dunia imejaaTAMAA YA MWILI, TAMAA YA MACHO NA KISHA KIBURI CHA UZIMA. Tamaa ina nguvu ya kuvuta pamoja na kudanganya, naam inamuingiza mtu kwenye jaribu. Hii ina maana tamaa ni mlango, naam mlango huu unapaswa kufungwa mapema usikupoteze.
(Samweli 11:1-2). Hapa Tunaona anguko la Daudi lilisaabishwa na kumpa Ibilisi nafasi kwa kutokwenda vitani. Mkristo akipoa katika kuvipiga vita vya kiroho inakuwa rahisi kwake kuanguka dhambini (Yakobo 1:14-15), na kumbuka kwamba siku zote tamaa inalenga kumfurahisha mtu binafsi (self-pleasing) bila kujali matokeo yake.
Hivyo katika nyakati tulizonazo sasa suala la kuipenda dunia ni lazima litafutiwe ufumbuzi wa kudumu miongoni mwa vijana wetu. Ujumbe huu mfupi unalenga kueleza kwa namna gani kuipenda dunia kumekuwa tanzi kwa vijana na nini vijana wafanye ili kuikabili na kuishinda changamoto husika.
Pia katika 2Timotheo 2:15 Mtume Paulo anaendelea kumwambia kijana Timotheo ‘Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa na Mungu,mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno la kweli’.
Pengine kila mmoja wetu atafakari maisha yake kwa kuhusianisha na maelekezo ya Paulo kwa Timotheo. Naomba jiulize na kujijibu kwa uaminifu kwamba mosi, je, ujana wako wako unaheshimika au unadharauliwa? Pili, je, kwa waamini wenzako umekuwa kielelezo cha kweli kwa habari ya imani, upendo, usafi, usemi na mwenendo au la?
Naam katika kusoma na kutafakari neno la Mungu nimejifunza kwamba zifuatazo ni njia ambazo zitatusaidia sisi vijana wa leo kuifikia kweli hii ya neno la Mungu.
1. Kijana adumu katika kuomba na kusoma (kutafakari + kulitenda) neno la Mungu.
Katika Zaburi 119:9 & 11 Biblia inasema ‘Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii AKILIFUATA neno lako’. Pia kwenye ule mstari wa 11 inasema ‘moyoni mwangu nimeliweka neno lako, NISIJE NIKAKUTENDA DHAMBI’.
Naam katika Mathayo 26:41 imeandikwa ‘Kesheni, mwombe, MSIJEmkaingia majaribuni; roho I radhi, lakini mwili ni dhaifu’. Yohana 17:17 inasema ‘uwatakase kwa ile kweli ;neno lako ndiyo kweli. Mambo haya mawili yanapaswa kwenda kwa pamoja nakijana akidumu katika kuomba na kusoma neno la Mungu ushindi ni lazima.
2. Kijana asimpe Ibilisi nafasi.
Kijana anapaswa kujiuepusha na mazingira yenye kumfanya aiepende na kuifuatisha namna ya dunia hii.
Katika kitabu cha 1Wakorinto 6:12 imeandikwa ‘Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote VIFAAVYO; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya UWEZO wa kitu chochote’. Ni vizuri ukahakikisha kwamba ufahamu wako hautawaliwi na mambo yasiyo ya msingi– Je ufahamu wako umetawaliwa ni nini??
Hii ndiyo sababu iliyomfanya Paulo awaambie Waefeso ‘Wala msimpe Ibilisi nafasi’ (Waefeso 4:27) na pia awaambie Warumi “Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili hata kuwasha tamaa zake’ (Warumi 13:14).
➡ Je hivi leo ni kwa namna gani vijana wanaungalia mwili na kumpa Ibilisi nafasi? – Mitandao ya kijamii, kuangalia na kusoma vitu vichafu, hasira, mawazo, mazingira.
Mfano wa Vijana
3. Kijana azikimbie tamaa za ujanani.
Katika 2Timotheo 2:22 imeandikwa ‘LAKINI ZIKIMBIE TAMAA ZA UJANANI; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi’. Kijana anawezaje kuzikimbia tama za ujanani?angalia mfano wa Yusufu. Ushindi wa Yusufu dhidi ya mke wa potifa (Mwanzo 39:2-9).
Hii ni habari ya kijana Yusufu ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa mali za Potifa.
Pamoja na ushawishi aliokutana nao Yusufu alijibu kwamba ‘Nifanyeje ubaya huu mkubwa nikamkose Mungu?’ Mwanzo 39:12 inasema ‘huyo mwanamke akamshika nguo zake, akisema, Lala nami. Yusufu akaiacha nguo yake mkononi mwake akakimbia akatoka nje. Ili kuzikimbia tamaa za ujanani kijana anapswa,
(a) ajiepushe na mazingira/marafiki wabaya (Mithali 1:10 & 1Wakorinto 15:33).
(b) Ajitenge na uovu (Mithali 16:17, Zaburi 1:1).
Ni muhimu ukakumbuka kwamba hukupewa mwili kwa ajili ya zinaa maana miili yenu ni ni viungo vya Kristo na tena hekalu la Roho Mtakatifu (1 Wakorinto 6:15 & 19), tena yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye (1 Wakorinto 6:17) maana tena imeandikwa ‘Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili’ (1Wakorinto 6:13b). Tena imeandikwa ‘Lakini uasherati USITAJWE kwenu kamwe, wala uchafu wowote wa kutamani, kama iwastahilivyo watakatifu’ (Waefeso 5:3)
Rafiki, mkimbilie Yesu leo akuwezeshe kuishi maisha yanayompendeza maana unazo nguvu za kumshinda ibilisi.
BWANA AWABARIKI SANA.
Na Isaiah membe, mtumwa wa Kristo.